Mapigano yameanza upya jana nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kati ya jeshi la kundi la waasi wa M23, siku moja baada ya watu wengi kukimbia maeneo yanayodhibitiwa na waasi yanayoshambuliwa na ndege za jeshi.
Wakaazi wameliambia shirika la habari la AFP kwamba walisikia sauti za mapigano zaidi kufikia jioni, baada ya kimya cha siku nzima. Maafisa walisema Jumanne kwamba jeshi la DRC lilitumia ndege kushambulia maeneo ya M23 mashariki mwa nchi, huku baadhi ya wakaazi wakikimbilia nje ya mpaka.
Wakati mapigano yakipamba moto, mji wa Rugari unadhaniwa kuwa karibu na msitari wa mbele wa mapambano, kilomita 30 kutoka mji wa Goma. Umoja wa Mataifa umesema jana kuwa watu wasiopungua 188,000 wamekimbia vijiji vyao tangu Oktoba 20, yalipoanza mashambulizi mapya ya M23, ambapo alau 16,500 wamejihifadhi katika nchi jirani ya Uganda.