Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, amesimamia mwenyewe majaribio ya makombora ya masafa marefu aliyoyaelezea kuwa ni mafanikio ya kupanuka kwa mpango wake wa nyuklia na kukua kwa uwezo wa jeshi lake ambalo liko tayari kwa kile alichokiita "vita halisi".
Majaribio ya hapo jana yameongeza idadi ya maonyesho ya silaha za Korea Kaskazini katika mwaka huu ambapo nchi hiyo imekuwa ikitoa matamshi ya kutumia silaha za nyuklia ili kujilinda na vitisho vya Marekani na Korea Kusini.
Wadadisi wa maswala ya kisiasa wanasema Kim anatumia fursa hii ambayo macho ya ulimwengu yameelekezwa katika mzozo wa Urusi na Ukraine, ili kufanikisha kwa haraka mpango wake wa silaha za nyuklia, ambazo zitakua tishio kubwa kwa Marekani na washirika wake wa kikanda.