India yasimamisha kiwanda cha dawa iliyouwa watoto nchini Gambia

Mamlaka nchini India imesimamisha kazi za kiwanda kilichotengeneza dawa inayochunguzwa, ikishukiwa kusababisha vifo vya watoto 69 nchini Gambia. Shirika la Afya Ulimwenguni WHO lilitoa tahadhari wiki iliyopita, kwamba dawa ya kikohozi na mafua inayotengenezwa na kiwanda cha Maiden Pharmaceuticals kilichoko katika jimbo la Haryana la kaskazini mwa India, inaweza kusababisha madhara makubwa kwenye maini.

Vipimo vya maabara vilibaini kuwa dawa hiyo ina kiwango kisichokubalika cha kemikali hatari kwa maisha, na WHO imesema kwamba imeuzwa nje ya Afrika Magharibi.

Waziri wa afya wa jimbo la Haryana Anil Vij amesema wametoa amri ya kusimamishwa mara moja utengenezaji wa dawa zote katika kiwanda kinachohusika, na kuongeza kuwa uchunguzi wao umegundua visa 12 vya ukiukaji wa kanuni katika kiwanda cha Maiden.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii