Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amesema kuwa karibu wasafiri wote waliokuwa katika boti iliyopinduka kwenye mto Niger wamekufa. Wafanyakazi wa huduma za uokozi wa dharura wamekwishathibitisha vifo vya watu 76 kati ya 85 wanaoripotiwa kuwa katika boti hiyo ilipopata ajali.
Taarifa ya Ikulu ya Rais Buhari imemnukuu kiongozi huyo akiwaombea dua waliopoteza maisha na kuzitakia afueni familia zilizopoteza wapendwa wao, na kuhimiza idara zinazohusika kuzifariji familia hizo.
Mratibu wa huduma za dharura ngazi ya taifa kusini mwa Nigeria Thickman Tanimu amesema kuongezeka sana kwa kina cha maji ya mto Niger katika eneo la Ogbaru kumetatiza shughuli za uokozi. Boti hiyo ilipinduka Ijumaa iliyopita.
Ajali za majini hutokea mara kwa mara nchini Nigeria, kutokana na vyombo kupakia kuliko uwezo wake, kasi kubwa, uchakavu wa vyombo hivyo na kutojali kanuni za usafiri wa majini.