Watumishi KCMC kwa makosa ya kimtandao

Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro, kitengo cha makosa ya kimtandao, linawahoji wafanyakazi kadhaa wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC ya mjini Moshi kwa tuhuma za makosa mbalimbali ya kimtandao.


Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Simon Maigwa ambaye yuko safarini kikazi nje ya mkoa, alipoulizwa juzi alithibitisha kuwapo kwa uchunguzi, lakini hawezi kutoa taarifa za uchunguzi huo kwa sasa.

“Niko nje ya mkoa, lakini hata hivyo unatoaje taarifa ambayo uchunguzi wake unaendelea na bado kukamilika?” alisema Kamanda Maigwa kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) aliomtumia mwandishi wetu kwa njia ya Whatsapp.


Taarifa za baadhi ya wale wanaotajwa kuhojiwa au kutafutwa na polisi kwa ajili ya mahojiano hayo, zinadai kiini cha tatizo hilo kilianzia kwa wafanyakazi wanaodai posho ya kufanya kazi saa za ziada, ambayo ni malimbikizo ya miezi mitatu.

“Ila jambo lipo hivi hapa KCMC sisi wafanyakazi hatulipwi hela zetu za overtime (saa za ziada) na hela ya bima kwa wakati. Jambo hili likatulazimu kufungua space huku Twitter mara kadhaa na kuwasema hospitali ili watulipe stahiki zetu”

“Hili limefanya wao wanaona yanayoendelea juu ya hospitali yao ikawauma na kuanza kuwatumia mapolisi kuanza kutafuta na kuhoji ni akina nani walioanzisha jambo hili huku mitandaoni,”unaeleza ujumbe wa mmoja wa wafanyakazi hao.Alipotafutwa na gazeti hili jana, Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Gabriel Chisseo alikiri kuwa na taarifa ya baadhi ya wafanyakazi kuhojiwa na polisi kwa matendo, ambayo alisema hayahusiani na madai yao, na kwamba madai yao yanashughulikiwa.




Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii