Aliyemuua Mkatisha Tiketi za Mabasi Ahukumiwa kunyongwa hadi Kufa
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu kunyongwa hadi kufa mshitakiwa Hemed Ally baada ya kupatikana na hatia ya kumuua, Farhani Maluni ambaye alikuwa mkatisha tiketi za mabasi ya kampuni ya waida aliyeuawa Juni 12, 2014 katika eneo la Sharifu Shamba Ilala, Dar es Salaam na kumzika mbele ya nyumba aliyokuwa amepanga.
Akisoma hukumu hiyo kwa saa mbili, Hakimu Mkazi Mkuu, Joyce Minde, amesema upande wa mashitaka ulipeleka mahakamani hapo mashahidi wasiopungua 12 na vielelezo ikiwamo hati ya amri ya kufukuliwa kwa mwili wa marehemu baada ya kupitia ushahidi wote, aliridhika kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo kwa makusudi.
Amesema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ulikuwa wa kimazingira, lakini umeweza kuthibitisha kwamba Ally alikuwa na nia ya kuua kutokana na kushindwa kununua gari aina ya Fusso, licha ya marehemu kumpatia Sh milioni 30.
Hakimu Minde amesema ni lazima mahakama ijiridhishe kwa asilimia 100 endapo kuna ushahidi wa mazingira bila kuacha shaka yoyote kwamba kilichotokea ndiyo uhalisia, hivyo mahakama imejiridhisha kuwa mshitakiwa alikuwa ana nia ovu.

Ndugu wakiangua vilio baada ya kutolewa hukumu hiyo.
Nikimnukuu hakimu alisema kuwa “Upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha kuwa kitu kilichofukuliwa Februari 9, 2015 eneo la Sharifu Shamba Ilala, Dar es Salaam kilikuwa ni mabaki ya mwili wa binadamu pia waliweza kuthibitisha kupitia daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu na vifo vya mashaka, Innocent Mosha, aliyeeleza kwamba marehemu Maluni kabla ya kuuawa na kufukiwa, alifungwa kamba ya katani mikononi na kichwani pamoja na plasta,” alisema Hakimu Minde.
Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Minde alisema uthibitisho wa masalia ya marehemu yalithibitishwa kutokana na nguo za marehemu zilizopatikana kwenye mabaki hayo ambazo zilithibitishwa na mke wa marehemu, Tatu Ally ambaye alidai ndiyo nguo alizomuandalia mumewe.
Akielezea hoja ya upande wa mtuhumiwa amesema kuwa mshitakiwa hakuweza kuleta ushahidi mahakamani kama alihama kwenye nyumba aliyopanga Sharifu Shamba kwa sababu ya maji na umeme kuunganishwa kinyume cha sheria.
Baada ya kuelezwa hivyo, Hakimu Minde alimueleza mshitakiwa kuwa adhabu yake kwa mujibu wa sheria ni kunyongwa hadi kufa hivyo akafunga hukumu na kuchukuliwa na polisi kuelekea gerezani.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Ally alikubaliana na Farhani (marehemu) kumnunulia gari aina ya Fusso na alikabidhiwa Sh milioni 30 lakini alishindwa kumkabidhi gari na alipanga njama za kuua.
Nje ya Mahakama ya kisutu baada ya hukumu hiyo Mke wa marehemu, Maluni, Tatu Ally akiwa na ndugu wengine alikuwa akilia kwa uchungu huku akisema Mahakama imetenda haki kwa sababu mshitakiwa amemtenganisha mume wake na watoto wake wawili.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii