Watu 45 wadakwa operesheni maalumu Kigamboni

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa amesema Jeshi la Polisi wilayani humo linawashirikia watu 45 katika operesheni maalumu ya kukabiliana na vitendo vya kihalifu.

Septemba 15, 2022 akizungumza na wenyeviti wa Serikali za mitaa na wajumbe kamati ya ulinzi na usalama ya Kigamboni, Nyangasa alitangaza kuanza kwa operesheni maalumu ya kukabiliana na vitendo vya kihalifuwakiwamo vijana wanaodaiwa kuwa ‘panya road‘ waliofanya uhalifu maeneo ya Kawe na Tabata.

Jana Jumamosi Septemba 17, akitoa tathimini fupi ya mwenendo wa operesheni hiyo, Nyangasa amesema, “operesheni inaendelea vizuri na watu 45 wanashikiliwa na polisi. Operesheni hii endelevu, tunaomba ushirikiano wa wananchi katika mchakato huu.

“Tupeni taarifa, shiriki katika ulinzi shirikishi, lengo ni kuhakikisha Kigamboni inaendelea kubaki salama kama maeneo mengine ikiwemo mkoa huu kwa ujumla. Nimetoa namba maalumu binafsi kwa ajili ya watu kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi utakaotusaidia kupata taarifa za viasharia vya uhalifu,”

Hata hivyo, Nyangasa amesema kwa wilaya ya Kigamboni bado hawajakumbana na vitendo vya panya road, lakini haiwafanyi wasijipange wala kuchukua tahadhari, ndio maana wameendesha operesheni maalumu.

Kwa siku za hivi karibuni kumeripotiwa matukio ya kihalifu maeneo ya mtaa wa Dovya Chamanzi, Wilaya ya Temeke ambapo vijana wakiwa na mapanga, nondo na marungu walivamia, kujeruhi na kuiba vitu mbalimbali vikiwemo simu, runinga na fedha.

Siku hiyo hiyo vijana hao walivamia maeneo ya Kawe Mzimuni, Dar es Salaam na kujeruhi, kupora mali na kusababisha kifo cha Maria Basso (24) mwanafunzi wa Shule ya Uandishi wa Habari Dar es Salaam (SJMC) ambaye amezikwa jana katika makuburi ya Mwenge.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni amesema hakuna

atakayejihusisha na uhalifu atabaki salama. Msimamo wa Masauni ulikuja baada ya juzi wabunge kuomba kuahirishwa kwa shughuli za Bunge kwa muda ili kujadili, kadhia ya vikundi vya uhalifu vinavyoundwa na vijana maarufu ‘panya road’ wanaovamia, kujeruhi na kupora mali mbalimbali

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii