Korea Kusini na Japan zimesema leo kuwa Korea Kaskazini imefyatua makombora mengine mawili, siku mbili tu baada ya jaribio lake la mwisho. Shirika la Habari la Korea Kusini, Yonhap limeripoti kuwa Korea Kaskazini imerusha makombora hayo kuelekea Bahari ya Japan, inayojulikana pia kama Bahari ya Mashariki.
Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida imesema makombora hayo ni ya masafa mafupi. Kishida amesema hii ni mara ya sita ndani ya siku 12 Korea Kaskazini inarusha makombora yake na kwamba jambo hilo haliwezi kuvumiliwa kabisa.
Korea Kaskazini imesema urushaji huo wa makombora ni katika kukabiliana na luteka za kijeshi za Marekani na Korea Kusini. Makombora hayo yamerushwa wakati ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kuzungumzia jaribio la kombora la Korea Kaskazini kuelekea Japan siku ya Jumanne.