Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia mkazi wa Manispaa, Mohamed Njali, kwa tuhuma za kumdhalilisha kijinsia mama mjamzito, Atka Kivenule na kumsababishia kifo chake.
Tukio hilo limetokea Jumamosi usiku mtaa wa Maweni, kata ya Kitazini/Myomboni ambapo mtuhumiwa huyo alivamia nyumbani kwa Adeline Kileo, saa 5 usiku.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Allan Bukumbi, alikiri kutokea kwa tukio hilo na wanaendelea na uchunguzi ili kujua sababu za mauaji hayo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Alfred Mwakalebela amethibitisha kupokea mwili wa mwanamke anayedaiwa kubakwa hadi kufariki akiwa na ujauzito wa wiki 10.
“Inasemekana alikuwa amelala ndani akavamiwa na mtu na katika uchunguzi tumegundua alivunjwa koromeo tulikuta michubuko inaonekana mbakaji alikuwa akimnyonga shingo ili atimize azma yake,’ alisema Mwakalebela.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kutokea tukio hilo na kwamba, uchunguzi zaidi unaendelea.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Moyo alisema mtuhumiwa amekamatwa na kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa hatua zaidi.
Moyo alisema hajafurahishwa na matukio ya ukatili yanayoendelea mkoani hapo na kusema inahitajika nguvu ya pamoja kati ya Serikali, wananchi na wadau mbalimbali katika kupiga vita matendo hayo ya udhalilishaji wa kijinsia.