Padri Mbaroni Kwa Kulawiti Watoto 10

Vitendo vya udhalilishaji wa kingono kwa watoto vinazidi kuitikisa nchi na sasa padri mmoja wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwabaka na kuwalawiti watoto zaidi ya 10.

 Watoto hao ni wanafunzi wa kuanzia darasa la sita hadi kidato cha kwanza waliokuwa wakihudhuria mafundisho ya komunio ya kwanza na kipaimara.

Inadaiwa kila alipomaliza haja zake, padri huyo humpa kila mmoja kati ya Sh3, 000 na Sh5,000.

Wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, akikataa kuthibitisha au kukanusha kukamatwa kwa padri huyo, Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu amethibitisha uwepo wa tukio hilo alilosema “ni baya linalofedhehesha”.

Tukio hilo ambalo ni la kwanza kusikika likifanywa na kiongozi wa dini mkoani Kilimanjaro, huku likihusisha idadi kubwa ya wanafunzi, limeibua taharuki kwa wazazi na walikuwa wamejipanga kuandamana kwenda kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wananchi hao walikuwa wamepanga kuandamana kwenda kwa Waziri Mkuu aliyekuwa mgeni rasmi katika Siku ya Amani Duniani ambayo kitaifa ilifanyika mjini Moshi, ili kupaza sauti zao kutokana na kigugumizi cha kukamatwa kwa padri huyo.

Baada ya polisi kupata fununu za wazazi kujipanga kuandamana na mabango kwenda kwa Waziri Mkuu, ndipo jioni ya Septemba 20, siku moja kabla ya kiongozi huyo kuwasili mkoani Kilimanjaro, walikwenda kumkamata.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alipotafutwa juzi ofisini kwake kuzungumzia uwepo wa tukio hilo, alikataa kuthibitisha au kukanusha kukamatwa kwa padri huyo zaidi ya kusema wanaendelea kuchunguza tukio hilo.

“Siwezi kusema kama tumemkamata au hatujamkamata, ila suala hili tunaendelea kulichunguza ili kujua ukweli wake, kwa sababu tuhuma hizi zinaelekezwa kwa kiongozi wa dini, hatuwezi kukurupuka kutoa taarifa,” alisema Maigwa.

Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, zinadai kuwa baada ya wazazi, kubaini watoto wao kufanyiwa vitendo hivyo, walitoa taarifa hizo kwenye vyombo husika ikiwemo uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi na Polisi.

Jina la padri huyo na kituo chake cha kazi tunavihifadhi kwa sasa kwa sababu za kimaadili, hasa kwa kuwa hatujapata upande wake wala vyombo vinavyomshikilia.

Jana, gazeti hili lilimtafuta kwa simu Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Ludovick Minde na baada ya kuulizwa taarifa za padri huyo, alisema wapo katika kipindi cha sala, hivyo asingeweza kuzungumza chochote kwa wakati huo (ilikuwa saa 7:12 mchana).

Ilipofika saa 10 jioni Mwananchi, lilimpigia tena simu Askofu Minde ambapo ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

Hata hivyo, Mkuu wa mkoa Babu alisema tukio hilo lipo na kwamba ameviagiza vyombo vya usalama kwamba mtu yeyote atakayekamatwa kwa matukio hayo na ushahidi upo, hakuna kurudi nyuma wanapaswa kuchukuliwa hatua kali.

“Katika tabia mbaya zisizo za watu waliostaarabika ni hizo, inaonekana mkoa wetu umezidi kuwa na matukio kama haya. Naviagiza vyombo vya usalama kwamba mtu yeyote atakayekamatwa na ushahidi upo hakuna kurudi nyuma,” alisema RC Babu.

“Kwa sababu haiwezekani kiongozi wa dini kama huyo afanye mambo kama hayo yanayofedhehesha hata waumini wake. Mambo kama haya kwa nchi yetu ni ya kuchafua taswira ya mkoa na nchi na nitaomba mahakama impe adhabu kali,” alisema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii