Macho Yote Sasa Kwa Majaji 7

Majaji saba wa Mahakama ya Upeo wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kutambua ukweli ulipo kwenye rundo la maelfu ya nakala za ushahidi ambao umewasilishwa mbele yao na wahusika kwenye kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9.

Kibarua hicho ni kigumu zaidi kwa majaji hao kwani wanahitajika kusikiliza kesi hiyo kuanzia kesho Jumatano na kutoa uamuzi wao Jumatatu ijayo kuhusu iwapo wanakubaliana na tangazo la IEBC kuwa William Ruto alichaguliwa rais kwa njia halali ama kuagiza marudio ya uchaguzi huo.

Wahusika kwenye kesi nane ambazo zimewasilishwa, kuu ikiwa ni ya mwaniaji wa Azimio Raila Odinga, washtakiwa ambao ni Dkt Ruto na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pamoja na wahusika wengine, wamejaza nakala katika mahakama hiyo zenye madai ya kila aina.

Hali hii inawaacha majaji Martha Koome, Philomena Mwilu, Njoki Ndung’u, Smokin Wanjala, Mohamed Ibrahim, Isaac Lenaola na William Ouko wakiwa na wakati mgumu kutenganisha ukweli, porojo na uwongo.

Msajili wa Mahakama ya Upeo, Letizia Wachira akipokea nakala za ushahidi kutoka kwa wahusika kwenye kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais. 

Kesi hiyo inayoanza leo Jumanne kwa kikao cha kuweka kanuni za kuiendesha ni ya kipekee kwani kwa mara ya kwanza makamishna wa IEBC wamegawanyika kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais.

Hii ni kinyume na 2013 na 2017.

Kambi hizo mbili za makamishna zimewasilisha hati za kiapo zinazoonyesha migawanyiko kwa misingi ya kisiasa.

Mrengo mmoja unashirikisha Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, Afisa Mkuu Hussein Marjan na makamishna Abdi Guliye na Boya Molu ambao wameomba mahakama kushikilia tangazo lao kuwa Dkt Ruto alishinda urais.

Mgawanyiko IEBC

Mrengo huo unasisitiza kuwa ulifuata kanuni na sheria za uchaguzi kikamilifu licha ya shinikizo kutoka kwa serikali na makamishna wenzao za kubatilisha matokeo.

Kambi ya pili inaongozwa na Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera anayeshirikiana na makamishna Justus Nyang’aya, Francis Wanderi na Irene Masit.

Makamishna hao wanne walioteuliwa Septemba 2021, wanadai matokeo ya uchaguzi wa urais yalivurugwa ili kumpendelea Dkt Ruto.

Hii ina maana kuwa jukumu la kwanza la Mahakama ya Upeo litakuwa ni kuamua ni kambi gani yenye mamlaka ya kujibu kesi hiyo kwa niaba ya IEBC.

Hapo jana Jumatatu Dkt Ruto aliwasilisha ombi la makamishna sita kuondolewa kwenye kesi hiyo akisema uchaguzi uliendeshwa na IEBC kama tume wala sio makamishna binafsi.

Kwa mara ya kwanza pia katika uchaguzi wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais, Mwanasheria Mkuu ametangaza kuwa hatapinga kesi hiyo isipokuwa moja ambayo imewasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, ambayo inapinga kesi ya Azimio.

Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki ameomba kuruhusiwa kushiriki kwenye kesi hiyo kama “Rafiki wa Mahakama”.

Baraza la Usalama wa Kitaifa (NSAC) pia limeomba kushirikishwa kwenye kesi hiyo.

Hii ni baada ya Bw Chebukati kudai kuwa maafisa wake walijaribu kushawishi IEBC kubatilisha matokeo ya urais. Baraza hilo litawakilishwa na Mwanasheria Mkuu kwenye kesi hiyo.

Kwenye shughuli ya kuweka kanuni za kuendesha kesi hiyo, ni mawakili wanne wa kila upande ambao watakubaliwa kushiriki.

Mbali na kesi ya Bw Odinga kuna nyingine ambazo zimewasilishwa na mwanaharakati Khelef Khalifa, Seneta Mteule wa Busia Okiya Omtatah, mwimbaji wa nyimbo za dini Reuben Kigame, taasisi ya Youth Advocacy Africa, John Njoroge Kamau, Juliah Nyokabi Chege na David Kariuki Ngari.

Inatarajiwa kuwa mahakama hiyo itaunganisha kesi hizo zote kuwa moja.

Kwenye kesi sawa mnamo 2013 mahakama hiyo ilitupilia mbali kesi ya Bw Odinga lakini 2017 ikafuta matokeo na kuagiza marudio, lakini Bw Odinga akakataa kushiriki.

    Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii