Uchaguzi wa Ugavana katika mji wa pwani ya Kenya wa Mombasa utafanyika Jumatatu ya Agosti 29. Kampeni za uchaguzi huo uliyoahirishwa mara mbili zinafikia tamati leo. Ushindani mkali katika nafasi hiyo utawakutanisha wagombea wawili Hassan Omar Sarai wa chama cha UDA ambaye aliwahi kuhudumu kama seneta wa Kaunti ya Mombasa na Abdul-Swamad Nassir wa chama ODM ambaye amehudumu kama mbunge wa Mvita. Tume huru ya uchaguzi na mipaka, IEBC, kupitia mwenyekiti wake, Wafula Chebukati, iliahirisha uchaguzi huo kutokana na vitisho na kunyanyaswa kwa maafisa wake. Jana Magavana wa kaunti zengine 45 waliapishwa huku Magavana wa Mombasa na Kakamega wakisubiriwa kupatikana.