Mshukiwa wa pili wa mashambulizi ya visu Canada afariki dunia

Mshukiwa wa pili aliyekuwa anasakwa na polisi ya Canada kufuatia mashambulizi ya kutumia visu mwishoni mwa wiki iliyopita ambayo yaliwauwa watu 10 katika eneo la jamii ya watu wa asili la Saskatchewan amefariki dunia. Shirika la Habari la Canada la Global News limeripoti kuwa mshukiwa huyo alifariki kutokana na majeraha ya kujiumiza mwenyewe, muda mfupi baada ya kukamatwa. Polisi ya Canada awali ilisema kuwa Myles Sanderson mwenye umri wa miaka 30, alikamatwa karibu na mji wa Rosthern, Saskatchewan, karibu kilomita 100 kusini magharibi ya eneo ambalo mashambulizi hayo mabaya kabisa kuwahi kutokea katika historia ya nchi hiyo yalifanyika Jumapili. Global News ikitaja duru kadhaa za polisi imeripoti kuwa Sanderson alijisalimisha kwa polisi na akachukuliwa na gari la wagonjwa baada ya polisi kuligonga gari alilokuwa akiendesha. Kaka yake mkubwa, Damien Sanderson, mwenye umri wa miaka 31, alipatikana akiwa amekufa Jumatatu karibu na eneo la mashambulizi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii