Watu wasiopungua saba wamekufa hii leo baada ya tetemeko la ardhi kuupiga mji wa Kangding ulio katika jimbo la kusini magharibi mwa China la Sichuan. Tetemeko hilo la ukubwa wa 6.6 katika kipimo cha Richter lilisambaa hadi umbali wa kilometa 43 na kuharibu majengo pamoja na kuyaacha maeneo mengine bila nishati ya umeme. Mitetemo pia iliyatikisa majengo kwenye mji mkuu wa jimbo la Sichuan, Chengdu ambako mamilioni ya watu wamefungiwa majumbani chini ya vizuizi vikali vya kukabiliana na virusi vya corona. Mamia ya waokoaji wametumwa kwenda eneo ambalo ni kitovu cha tetemeko hilo huku wafanyakazi wengine wakijaribu kusafisha barabara zilizozuiwa na vifusi vya udongo ulioporomoka kutoka milimani.