Shambulio hilo lilitokea usiku wa Ijumaa kuamkia Jumamosi, na kuua takriban raia 19, kulingana na ripoti ya hivi punde. Wiki mbili zilizopita, hoteli moja katika mji mkuu, Mogadishu, ililengwa na mashaambulizi ya kundi hili la wanamgambo wa Kiislamu.
Washambuliaji walisimamisha mabasi madogo na malori yaliyokuwa yakisafiri pande zote mbili kwenye barabara inayounganisha miji ya Beledweyne na Maxaas. Takriban magari manane, ambayo wanamgambo hao waliyaweka sehemu moja na kuyachoma moto, baada ya kuwaua abiria waliokuemo ndani ya magari hayo. Vyanzo kutoka eneo hilo vinadai kuwa watu kadhaa pia walitekwa nyara.
Katika ujumbe wao wa kudai kuhusika katika shambulio hilo, Al-Shabab wanaeleza kwamba waliwashambulia wapiganaji ambao walisaidia vikosi vya serikali kupigana nao. Kufikia mwisho wa mwezi Agosti, vikosi vya usalama na wapiganaji wa ndani walikuwa wamedhibiti tena vijiji kadhaa katika eneo hili la Somalia.
Rais wa Somalia Jumamosi jioni alilaani vitendo vya kuchukiza kwa raia wasio na hatia. Hassan Cheikh Mohamoud, ambaye amekabiliwa na kuzuka upya kwa shughuli za Al-Shabab tangu kuchaguliwa kwake mwezi Mei mwaka jana, ameahidi kwamba serikali haitapuuzia juhudi zozote katika vita dhidi ya ugaidi.
Wiki mbili zilizopita, hoteli kubwa katika mji mkuu, Mogadishu, ililengwa. Shambulio hilo lililodumu kwa takriban saa 30, lilisababisha vifo vya watu 21 na wengine 117 kujeruhiwa.