Mamlaka nchini Mali zimetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanza leo, baada ya mashambulizi mawili yaliyofanywa na makundi ya Kiislamu yenye msimamo mkali kusababisha mauaji ya wanajeshi na polisi. Jeshi la Mali lilisema kwamba shambulio la Jumapili katika mkoa wa kaskazini wa Gao, liliwaua askari 42. Maafisa wengine watano wa polisi waliuawa katika shambulizi jingine la kusini mwa nchi, baada ya wanamgambo wenye misimamo mikali kukishambulia kituo cha polisi karibu na mpaka na Burkina Faso. Mali na washirika wake wa kimataifa wamekuwa wakikabiliana na wapiganaji wenye itikadi kali kwa karibu muongo mmoja. Mapambano hayo yanaonekana kuzorota baada ya Ufaransa kuanza kuondoa vikosi vyake kufuatia tofauti na serikali ya Mali. Mwaka 2013, Ufaransa iliongoza operesheni za kijeshi kuwafurusha wanamgambo katika miji mikubwa ya Kaskazini.