IEBC yawataka Wakenya kuwa watulivu wakati kura zikiendelea kuhesabiwa.

Wakenya kwa siku ya pili leo, bado wanasubiri matokeo ya uchaguzi wa urais, baada ya kupiga kura siku ya Jumanne. Maafisa wa tume huru ya uchaguzi na mipaka ya Kenya IEBC, wameendelea na zoezi la kuhesabu kura huku tume hiyo ikikabiliwa na shinikizo la kutangaza matokeo kufikia Agosti 16.

Matokeo yanayoendelea kurushwa na vyombo vya Habari nchini humo yanaonesha kuwa kuna ushindani mkali kati ya naibu rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. 

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi anatarajiwa kuzungumza asubuhi hii. 

Tume itatangaza matokeo rasmi ya mwisho ya uchaguzi wa urais baada ya kuthibitisha fomu 46,229 zilizowasilishwa kutoka katika vituo vya kupiga kura kote nchini. Kuthibitishwa kwa matokeo haya kunaweza kuchukua siku kadhaa.

Tume hiyo ina hadi Agosti 16 kutangaza matokeo ya mwisho. Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati amewaomba Wakenya kuwa watulivu wakati shughuli ya kujumlisha kura ikiendelea, kuepuka madai ya udanganyifu wa kura ambayo yaligubika chaguzi zilizopita.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii