Raila Ashinda Kesi Kuhusu Utumizi Wa Daftari

KINARA wa Azimio Raila Odinga alipata ushindi mkubwa baada ya Mahakama Kuu kuamuru Alhamisi  daftari la sajili ya wapiga kura litumike wakati wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Uamuzi huu umekuwa pigo kubwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliyokuwa imeamuru wapiga kura watambuliwe kwa sajili ya kielektroniki.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, mfumo wa kutambua wapiga kura kielektroniki ulilenga kukwepa dosari ambazo zinaweza zikatokea wakati wa kupiga kura.

Jaji Mugure Thande alisema agizo hilo la IEBC ni kinyume cha katiba inayotaka kila mpiga kura atambuliwe katika sajili hivyo linakiuka haki za wapiga kura za kutambuliwa ipasavyo.

Jaji huyo alisema IEBC ilikosea kutangaza itaachana na sajili iliyoitayarisha kupiga chapa ikionyesha majina ya wapiga kura wote.

Jaji Thande alisema ni kutokana na sajili hii ya daftari ambapo ile ya kielektroniki ilitayarishwa.

“Utaratibu muwafa ni kwamba pale ambapo sajili ya kielektronik imekumbwa na dosari sajili ya daftari itumike,”alisema Jaji Thande.

Kuhusu sisitizo ya IEBC kwamba sajili ya kielektronik almaarufu KIEMS ndiyo itakayotumika, jaji huyo alihoji jinsi maafisa wa tume watakavyofanya endapo sajili ya kielektronik itakapokosa kuonyesha taarifa za mpiga kura.

Hofu kuu ya IEBC ilikuwa ni kuvurugwa kwa sajili ya daftari, ndipo ikaamua kutumia Kiems kuwatambua wapiga kura 22.1milioni.

IEBC iliungwa mkono katika utumizi wa Kiems na mwaniaji urais wa muungano wa Kenya Kwanza William Ruto.

Chama cha Ruto cha United Democratic Alliance (UDA) kilisema kuwa Kiems zitahakikisha hakuna wizi wa kura.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema tume iliamua kutumia Kiems kufuatia uamuzi wa mahakama ya juu kuhusu matokeo ya kura za urais.

Chebukati alisema kuwa tume pia ilitegemea ripoti ya jopo iliyoteuliwa kuchunguza ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Mwenyekiti huyo wa IEBC alisema  sajili ya daftari ilitumiwa vibaya nakupelekea kura kuibwa.

“Ili kuhakikisha ukora hauchipuki tena IEBC iliamua kutumia Kiems kuwatambua wapiga kura na kuhakikisha haki imetendeka,” alisema Chebukati.

UDA ilieleza korti IEBC inatakiwa kutumia mfumo muwafaka wa kuwatambua wapiga kura usiozua kiwewe.

 “Utumizi wa sajili ya daftari sio mfumo wa kufutilia mbali sajili ya Kiems,” alisema Jaji Thande.

Sajili hii ya daftari itafaa mahala ambapo hakuna Kiems.



    Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii