MPLA yashinda uchaguzi mkuu, kulingana na matokeo ya muda.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa matokeo yake ya hivi punde Alhamisi jioni. Tayari wamehesabu 97% ya kura. Kwa mara ya kwanza tangu uhuru, chama cha MPLA kimeshinda kwa kura ndogo.


Ilikuwa ni mapema jioni ambapo Lucas Quilunda, msemaji wa CNE, Tume Huru ya Uchaguzi, alitangaza matokeo. "Chama cha MPLA kina 51.7% ya kura, ambazo zinakiwezesha kuwa na wabunge 124. Chama cha Unita kina 44.5% ya kura na kuweza kupata viti 90 katika Bunge. Vyama vingine sita vya siasa vinagawana kura zinazosalia. Vinne kati ya vyamahivyo sita, kura walizopata haziwaruhusu kupata mbunge hata mmoja katika Baraza la Wawakilishi.

Pamoja na kura 10% pungufu kuliko katika uchaguzi wa 2017, chama cha MPLA kinapoteza wingi wake kamili wa kura katika Bunge. Kwa hivyo kitalazimika kukabiliana na upinzani, jambo ambalo halimsumbui Rui Falcao, msemaji wa MPLA. "Haibadilishi chochote, sio kikwazo kwa kuliongoza taifa. Tunahitaji kuchukua muda kuchanganua yaliyotokea, safari yetu katika kipindi cha miaka 5 iliyopita na, kwa kuzingatia hili, kuelekeza upya baadhi ya matendo yetu. Wananchi wanataka tutawale kwa wingi kamili, na ndivyo tutakavyofanya. "

Wafuasi wa chama cha Unita, kwa upande mwingine, hawaonekani kuwa tayari kuafikiana. Mbele ya makao makuu ya chama, katika wilaya ya Vienna, hasira inazidi kupanda. "Sisi kama watu tuna hakika kuwa matokeo haya si ya kutegemewa. Chama cha MPLA kimeshindwa, ni wakati wa Joao Lourenço kuondoka ikulu. Chama cha MPLA kilnashindwa kila mara. Kila mara kinaposhinda, si kwa sababu ya kitu kingine. Hatutaki ulaghai wowote. Tutaomba haki zetu kwa amani, sisi si waharibifu, hatutaki machafuko. Tutafanya kile tunachoruhusiwa na sheria, tena kwa utulivu. "

Mgombea wa chama cha Unita Adalberto Costa Junior bado hajazungumza. Lakini matokeo haya ni ya kukatisha tamaa chama. Alhamisi hii alasiri, chama kilikuwa kimetangaza hesabu yake, kwamba chama cha MPLA na chama cha Unita walikuwa wakikaribiana kura, huku chama cha MPLA kikiwa na 47% na Unita kikiwa na 46% ya kura. Pengo ambalo chama cha upinzani kilikuwa na uhakika kingeweza kuziba.

Upinzani umelaani ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa uchaguzi tangu kuanza kwa kampeni. Mashtaka ambayo Rui Falcao, msemaji wa MPLA, alipuuzilia mbali. Siku ya Alhamisi hii jioni alikaribisha matokeo ya uchaguzi. Waangalizi kutoka Jumuiya ya nchi zinazozungumza Kireno, kwa upande wao, wamebaini kwamba chaguzi hizi zilifanyika "kulingana na matakwa ya kimataifa. "

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii