Rais wa Angola aongoza katika matokeo ya mapema ya uchaguzi

Angola inasubiri kwa hamu matokeo ya uchaguzi ulioshuhudia kinyangan'yiro kikali katika historia yao ya kidemokrasia. Matokeo ya mapema yanaonyesha rais wa sasa Joao Lourenco anaongoza lakini upinzani pia unadai kuwa unaongoza. Matokeo ya awali yaliyochapishwa leo asubuhi na tume ya uchaguzi ya Angola yamekipa chama tawala cha MPLA asilimia 52.08 ya kura huku asilimia 86.41 ya kura zikiwa zimekwisha hesabiwa. Chama kikuu cha upinzani cha UNITA kikiongozwa na kiongozi mkakamavu Adalberto Costa Junior kina asilimia 42.98. Lakini naibu kiongozi wa UNITA Abel Chivukuvuku amesema hesabu za chama hicho zinaonyesha kuwa kinaongoza. MPLA imeitawala Angola kwa karibu miaka 50 tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno. Zaidi ya watu milioni 14 walisajiliwa kupiga kura.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii