Waangola milioni 14 wanafanya Uchaguzi Mkuu Jumatano hii, Agosti 24 kumchagua rais wao mpya na wabunge. Vyama saba vya siasa na muungano vinashiriki kinyang'anyiro hiki.
Vita vya kuwania madaraka kwa mara nyingine tena vinashuhudiwa kati ya MPLA, chama cha Ukombozi wa Angola na UNITA, Umoja wa Kitaifa unaotetea Uhuru wa Jumla wa Angola, kambi mbili ambazo zimekuwa zikipigana kwa zaidi ya miaka 25 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Chama cha MPLA kimetawala bila kupingwa tangu uhuru wa nchi hiyo, lakini mchezo unaonekana kuwa wazi zaidi kwa Uchaguzi huu Mkuu.
"A hora, è agora ! " Wakati umewadia, anasema Aldaberto Costa Junior, mgombea anayepeperusha bendera ya chama cha UNITA, mbele ya maelfu ya wafuasi waliofika kumwona wakati wa mkutano wake wa mwisho, katika wilaya ya Cassenda.
Wakati huu chama cha UNITA kinaamini kuwa mabadiliko ya kisiasa yapo njiani. Adalberto Costa junior anajitambua mwenyewe, "ushindi" uko kwa ajili yake.
Akiwa na umri wa miaka 60, mwenye mvuto na mzungumzaji mzuri, alikua kiongozi wa chama cha UNITA mnamo 2019. Kwa kufuta sura ya waasi hao wa zamani, aliweza kupata uungwaji mkono wa sehemu kubwa ya vijana.
Adalberto Costa junior pia alikusanya vyama vingine vya upinzani kwa kuwania kwake. Miongoni mwa vyama hivyo ni pamoja na CASA-CE cha Abel Chivukuvuku, ambaye alipata 10% ya kura katika uchaguzi wa 2017.
Naye Joao Lourenço, rais anayeondoka madarakani yuko katika matatizo. Yule aliyeteuliwa na Jose Eduardo dos Santos kama mrithi wake, amekatishwa tamaa. Katika kipindi chote cha kampeni yake, ameangazia mafanikio yake na hasa rekodi yake ya kiuchumi: ujenzi wa miundombinu, kufungua soko, kutafuta wawekezaji wa kigeni... lakini maendeleo yaliyoahidiwa sana hayapo. Mbaya zaidi, nchi imekumbwa na athari za shida ya mafuta tangu mwaka 2016 na ile ya UVIKO-19. Leo hii 40% ya watu bado wanaishi katika umaskini uliokithiri.
Jambo lingine: mapambano yake dhidi ya rushwa. Joao Lourenço alifanya kuwa kipaumbele cha kampeni yake katika mwaka wa 2017. Ili kuonyesha uamuzi wake, aliongoza sakata dhidi ya familia ya Eduardo dos Santos, ambaye alimuona kama adui yake. Lakini operesheni hiyo haikuleta matokeo ya kisheria yaliyotarajiwa na wengi na kumtenga rais kutoka kwa sehemu ya taasisi za MPLA.
Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeidhinisha tu mwaka huu waangalizi 2,000 wa mashirika ya kiraia kufuatilia upigaji kura, kwa vituo 26,000 vya kupigia kura. Hii ndiyo sababu upinzani na mashirika ya kiraia yameanzisha vuguvugu la “voto, sento” (napiga kura, nabaki) ili kumtaka mpiga kura awe macho wakati wa zoezi la uhesabuji kura.