BARAZA la Vyombo vya Habari Nchini (MCK) sasa linasema kuwa uamuzi wa kusitisha uwasilishaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais moja kwa moja ulifikiwa baada ya vyombo vya habari kuonyesha matokeo tofauti.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Afisa Mkuu Mtendaji wa MCK David Omwoyo Jumanne, Agosti 23, 2022 alisema kuwa matokeo hayo kinzani yangeleta taharuki miongoni mwa Wakenya.
“Uamuzi wa kusitisha uwalishaji matokeo haswa katika runinga ulifikiwa na wadau katika sekta ya uanahabari wapohisi kuwa hatua hiyo ingeleta taharuki nchini. Uamuzi huo haukutokana na presha kutoka nje inavyodaiwa,” akasema katika ripoti hiyo.
Hata hivyo, Bw Omwoyo alisema matokeo ambayo yalikuwa yakionyesha yalikuwa “sahihi” kwa sababu yalitolewa kutoka mtandao (portal) wa IEBC.
“Lakini kwa sababu vyombo tofauti vya habari vilianza kuhesabu kura nyakati tofauti, na ukweli kwamba baadhi ya vyombo hivyo navyo viliajiri wafanyakazi wengi kuliko vingine na vingepata matokeo nyakati tofauti, matokeo hayakuwa sawa,” anaeleza.
MCK pia ilisema kuwa vyombo vya habari havingeshirikiana kukusanya matokeo kwa pamoja jinsi vilivyofanya kuandaa mdahalo wa urais, kwa sababu wazo hilo lilijiri “kuchelewa”.
“Japo wazo hilo lilikuwa bora, halikufikiriwa mapema. Lilipojiri, baadhi ya vyombo vya habari tayari vilikuwa vimetuma wafanyakazi/maajenti wao katika maeneo bunge kukusanya matokeo,” Bw Omwoyo anasema.
“Vile vile, vyombo vya habari vilipata fomu 34A kwa urahisi kwa sababu zilikuwa zimewekwa katika tovuti ya IEBC,” akaongeza.
Baada ya shughuli ya upigaji kura kukamilika mnamo Agosti 9, 2022 kura zilianza kuhesabiwa na matokeo kupeperushwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari.
Hata hivyo, baada ya siku moja vyombo hivyo, haswa televisheni, vilianza kutoa matokeo tofauti na yale ambayo yalikuwa yakitolewa kupitia tovuti ya IEBC. Hali hiyo iliibua maswali kuhusu uhalali wa matokeo hayo haswa miongoni mwa wafuasi wa wagombeaji wakuu wa urais Naibu Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.