Mwaniaji urais wa muungano wa Azimio Raila Odinga amedai Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka na Rais Mteule William Ruto walikula njama ya “kumpokonya ushindi” kwenye uchaguzi wa Agosti 9.
Kwenye nakala za kesi alizowasilisha Jumatatu katika Mahakama ya Juu kupinga kutangazwa kwa Dkt Ruto kuwa mshindi wa urais kwenye uchaguzi huo, Bw Odinga pamoja na mwenza wake Martha Karua wanasema njama hiyo ilianza miezi kadhaa iliyopita.
Wawili hao sasa wanataka Mahakama ya Juu kufutilia mbali kutangazwa kwa Dkt Ruto kuwa rais mteule na badala yake iagize kuhesabiwa upya kwa kura zote za urais, kisha kumtangaza Bw Odinga kuwa mshindi wa urais naye Bi Karua naibu wa rais.
Ombi lingine ambalo Bw Odinga na Bi Karua wametoa ni mahakama hiyo kuagiza marudio ya uchaguzi huo chini ya usimamizi mpya wa IEBC, kwani wanataka Bw Chebukati aondolewe wakisema “hawezi kusimamia uchaguzi huru na wa kikatiba”.
Katika maombi yao kwa Mahakama ya Juu, wawili hao wanasema uchaguzi wa Agosti 9 ulikumbwa na dosari nyingi ambazo “zinaufanya kukosa kufikisha viwango vya uchaguzi huru, wa haki, wazi na wa kikatiba”.
Kulingana na wawili hao, mgawanyiko baina ya makamishna wa IEBC ni ishara tosha kuwa tume hiyo haikuwa na uwezo wa kuendesha uchaguzi kikatiba na kisheria.
Hii ni kufuatia hatua ya makamishna wanne – Juliana Cherera, Justus Nyang’aya, Irene Massit na Francis Wanderi – kutofautiana na wenzao Chebukati, Boya Molu na Prof Abdi Guliye kuhusu takwimu za urais.
Wanne hao waliondoka katika ukumbi wa Bomas kabla ya Bw Chebukati kutangaza matokeo mnamo Agosti 15, na badala yake wakaelekea katika hoteli ya Serena walikotangaza kuwa hawakukubaliana na matokeo ambayo yalitangazwa ya mshindi wa urais.
Wanasema hii ni mara ya pili kwa Bw Chebukati kushindwa kufanya kazi na makanishna wenzake, kufuatia mazingira ya 2017 ambapo makamishna wanne walijiuzulu.
Hoja nyingine ambayo Bw Odinga na Bi Karua wanataja kama inayopasa kutumiwa kufutilia mbali ushindi wa Dkt Ruto ni kuwa hakufikisha asilimia 50 na kura moja ya jumla ya zilizopigwa.
Ubadilishaji kura
Wanadai kuwa kulikuwa na ubadilishaji wa kura kwenye Fomu 34A, ambapo wanasema kura za Bw Odinga zilikuwa zikifutwa na kuongezewa Dkt Ruto.
Pia wanasema hatua ya Bw Chebukati kutangaza matokeo ya urais kabla ya kutangaza matokeo ya maeneobunge 27 yaliyokuwa yamesalia kutangazwa ni sababu nyingine inayopasa kushawishi majaji wa Mahakama ya Juu kufutilia mbali ushindi wa Dkt Ruto.
Bw Odinga na Bi Karua pia wanadai mitambo ya IEBC ilikorogwa na kuna watu ambao waliweza kupenya na kubadilisha takwimu zilizokuwa kwenye fomu za matokeo ya kura za urais.
Wanadai kuwa mpango huo ulianza kabla ya uchaguzi, wakieleza kuwa raia wa Venezuela waliokamatwa nchini walikuwa sehemu ya njama hiyo ya “wizi wa kura”.
Sasa wanataka vifaa vilivyochukuliwa na polisi walipokamatwa pamoja na taarifa zao ziwasilishwe mahakamani kama ushahidi.
Tetesi nyingine wanayotoa ni kuwa katika ngome za Dkt Ruto za Rift Valley na Mlima Kenya kulikuwa na uongezaji wa kura kwa manufaa yake.
“Hii inaweza kufafanua hali ya Dkt Ruto kupata kura zaidi kuliko jumla ya zilizopigiwa wawaniaji wa viti vingine… Pia katika baadhi ya sehemu kulikuwa na wapiga kura zaidi ya walioandikishwa,” wanasema wawili hao.
Wanateta pia kuwa hatua ya kuahirisha uchaguzi wa ugavana wa Mombasa na Kakamega “ilikuwa njama ya kumhujumu Bw Odinga” wakisema kaunti hizo ni ngome zake, na kwa kuahirisha uchaguzi idadi ya wapiga kura ilipungua.
IEBC ilipoahirisha uchaguzi wa kaunti hizo ilisema kulikuwa na dosari kwenye karatasi za kiti cha ugavana.
Bw Odinga na Bi Karua wanalalamika pia kuwa kuharibika kwa mitambo ya KIEMS hasa katika kaunti za Kakamega na Makueni kulichangia kucheleweshwa kwa shughuli ya upigaji kura na hivyo kunyima wakazi fursa ya kumpigia kura Bw Odinga.
Wanasema kuwa kuna tofauti ya kura 140,028 kati ya wapiga kura waliotambuliwa kwa mitambo ya KIEMS na idadi iliyonakiliwa kwenye Fomu 34C.
Wanaeleza pia kuwa Bw Chebukati alijikanganya katika kutangaza idadi ya wapiga kura walioshiriki uchaguzi huo kwa kutoa taarifa tofauti, hivyo kuacha wengi bila kujua idadi kamili ya walioshiriki shughuli hiyo.