Mtu anayetuhumiwa kufadhili mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka wa 1994 Felicien Kabuga, atapandishwa kizimbani mjini The Hague Septemba 2. Jaji wa mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa Iain Bonomy amesema Kabuga atafunguliwa mashitaka ya mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Ameongeza kuwa ushahidi katika kesi hiyo utaanza kutolewa Oktoba 5. Mawakili wa Kabuga walitaka kesi hiyo ifutwe kwa misingi ya kiafya lakini mahakama hiyo ya The Hague ikakataa ombi hilo ikisema upande wa utetezi ulishindwa kuthibitisha kuhusu afya ya Kabuga. Mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 87 alikamatwa Mei 16 mwaka wa 2020 katika kitongoji cha mji mkuu wa Ufaransa Paris baada ya miaka 25 ya kuwa mafichoni.