Human Rights Watch yasema M23 imeuwa raia 29 wa Congo tangu katikati mwa Juni

Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limesema leo kuwa kundi la waasi wa M23 liliwatuhumu na kuwaua raia 29 pasina kuwapa fursa ya kujitetea tangu katikati mwa Juni, katika maeneo yalioko chini ya udhibiti wao. Shirika hilo limesema mashuhuda waliliambia kuwa Juni 21, kufuatia mapigano karibu na kijiji cha Ruvumu, M23 iliwauwa raia wasiopungua 17, wakiwemo watoto wawili, waliowatuhumu kwa kutoka taarifa kwa jeshi la Congo kuhusu ngome na maficho ya waasi hao. Limesema baadhi ya wahanga walipigwa risasi wakati wanajaribu kukimbia, huku wengine wakipigwa risasi kwa karibu. Vifo vingine vilitokea katika mashambulizi yaliofuatia kwenye kijiji sawa na katika vijiji vidogo vya Ruseke na Kabindi, na hivyo kufikisha idadi ya vifo kuwa 29. Mwezi uliyipita wapiganaji wa M23 waliuteka mji wa kimkakati wa Bunagana, kwenye mpaka wa Congo na Uganda. Serikali ya Congo inashtumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasiwa M23, madai ambayo serikali mjini Kigali inayakanusha.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii