Raia wa kigeni ambaye Alhamisi alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) nchini Kenya akiwa na stika za uchaguzi za Tume ya IEBC ameachiliwa kutoka kizuizini.
Siku ya Alhamisi, maafisa wa upelelezi kutoka DCI walianzisha uchunguzi baada ya lebo za tume ya uchaguzi kunaswa kutoka kwa abiria ambaye alikuwa amezificha kwenye begi lake la kusafiria.
Abiria huyo alikuwa na vifurushi 17 vya stika za kaunti mbalimbali za uchaguzi nchini.
Katika uchunguzi wao, polisi walitaka kuelewa kwa nini abiria alikuwa amebeba vifaa hivyo na ni nani aliyempa.
Msemaji wa Tume ya Huduma kwa Polisi Bruno Shioso alisema uchunguzi umebaini kuwa stika zilizopatikana ni mali ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Tume huru ya uchaguzi na mipaka ilikuwa imeelezea wasiwasi wake kuhusu kukamatwa na kuzuiliwa kwa wanakandarasi watatu wanaohusika na uwekaji na usimamizi wa miundomsingi ya teknolojia ya uchaguzi.
Katika taarifa, Tume hiyo , IEBC,ilisema wafanyikazi wa Smartmatic International B.V, walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta walipowasili kutoka Venezuela.
Tume hiyoilisema ilishangazwa kuwa hilo lilifanyika licha ya kuziarifu mamlaka za usalama kuwa watatu hao walikuwa nchini kihalali.
Mwenyekiti wa Tume Wafula Chebukati alisema kuwa kuendelea kuzuiliwa kungeweza kuathiri maandalizi ya uchaguzi kwani teknolojia ni kiungo muhimu katika uchaguzi wa Agosti.
'Tume ina mkataba halali uliotekelezwa kati yake na Smartmatic International B.V. kwa usambazaji, uwasilishaji, usakinishaji, majaribio , uagizaji, usaidizi na utengezaji wa Mfumo wa Kusimamia Uchaguzi wa Kenya' taarifa ya IEBC imesema