BI JUMWA APATA AHUENI KUHUSU DIGRII YAKE KUTUPWA

Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, amepata afueni baada ya Mahakama Kuu ya Mombasa kutupilia mbali ombi lililokuwa likitaka kumfungia nje ya kinyang’anyiro cha ugavana wa Kaunti ya Kilifi kwa madai ya kukosa digrii.

Jaji Stephen Githinji alifutilia mbali maombi mawili yaliyowasilishwa dhidi ya Bi Jumwa akisema mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo.

Jaji alikubali pingamizi la awali lililowasilishwa na Bi Jumwa, akisema waliowasilisha maombi walipaswa kufika kwanza kwenye Kamati ya Kusuluhisa Mizozo (DRC) ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kabla ya kukimbilia mahakamani.

Wakazi watatu wa Kilifi na shirika moja waliwasilisha kesi dhidi ya Bi Jumwa mwezi Juni, wakitaka kumzuia kuwania kiti cha ugavana wa kaunti hiyo.

Bw Karl Katingu, Bw Daniel Chengo, Rajab Menza na Concern Citizen Kenya, walipinga uteuzi na kutangazwa kwa mbunge huyo kama mgombea wa wadhifa huo kupitia kwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Uamuzi huo unamwacha Bi Jumwa bila mzozo wowote mwingine unaotilia shaka cheti chake cha masomo na huru kufanya kampeni zake bila woga.

Bi Jumwa anapambana na wakili George Kithi wa Pamoja African Alliance (PAA), Gideon Mung’aro (ODM), Dzombo Mbaru (Safina) na wagombea huru Michael Tinga na Francisco Esposito almaarufu Kasoso wa Baya.

Wagombea hao wameimarisha kampeni za kuwania kura 588,602 katika kaunti hiyo kumrithi Gavana Amason Kingi anayestaafu mwezi ujao.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii