Shirika la upelelezi la Marekani CIA, limesema takribani wanajeshi 15,000 wa Urusi wamekufa tangu Moscow ilipofanya uvamizi nchini Ukraine. Mkurugenzi wa CIA William Burns, amesema karibu idadi mara tatu ya wanajeshi wa Urusi wanaaminika kujeruhiwa tangu mwanzoni mwa vita, Februari 24. Burns ametoa makaridio hayo wakati wa mkutano wa usalama katika mji wa Aspen nchini Marekani. Amesema Ukraine imepoteza pia wanajeshi, lakini kwa idadi ya chini kuliko Urusi. Urusi haijaweka wazi takwimu mpya za vifo kuwa upande wake. Burns amesema katika mkutano huo wa jana usiku kwamba kulundikwa kwa wanajeshi wa Urusi katika kanda ya mashariki ya Donbas, inayojulimsha mikoa ya Luhansk na Donetsk, kunaashiria kwa sasa, kwamba jeshi la Urusi limejifunza kutokana na makosa yake mwanzoni mwa vita.