Naibu waziri wa ulinzi wa Ukraine Volodymyr Havrylov amesema nchi yake inaazimia kuishambulia rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi mwaka 2014, pamoja na jeshi la wanamaji wa Urusi walioko huko. Amesema Ukraine imepatiwa uwezo wa kuzishambulia meli, na ni suala la muda tu hadi watakapoanza operesheni hiyo. Akizungumza na gazeti la The Times akiwa ziarani mjini London, afisa huyo amesema ikiwa Urusi inataka kuendelea kuwepo kama taifa, itaibidi kujiondoa yenyewe kutoka Crimea. Akijibu kauli hiyo ya Havrylov, msemaji wa Ikulu ya Kremlin mjini Moscow, Dmitry Peskov amesema matamshi hayo yanathibitisha uhalali wa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, ambao Moscow inautaja kuwa ni operesheni maalumu ya kijeshi, na kuongeza kuwa ni hatua kama hiyo pekee inayoweza kuikomboa Ukraine kutoka kwa viongozi kama Havrylov.