Tume ya uchaguzi ya Pakistan imeamua leo kuwa chama cha Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan kilipokea fedha kwa njia haramu, hatua ambayo inaweza kusababisha nyota huyo wa zamani wa mchezo wa kriketi pamoja na chama chake kupigwa marufuku kujihusisha na siasa. Katika kesi ambayo imeendelea kwa miaka mingi, chama cha Khan kilituhumiwa kupokea fedha kutoka nje ya nchi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria nchini Pakistan. Khan hata hivyo hakupatikana kuzungumzia suala hilo lakini msemaji wa chama chake cha PTI amekanusha madai ya kuhusika na kupokea fedha hizo. Khan alihudumu kama Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2018 hadi Aprili mwaka huu alipolazimika kuachia ngazi baada ya kupoteza kura ya kutokuwa na imani na uongozi wake, japo alidai ilikuwa ni njama ya Marekani.