Lavrov apinga Urusi kubebeshwa dhima ya upungufu wa chakula duniani

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amepinga vikali madai kuwa nchi yake ndiyo inawajibika kwa kupanda kwa bei za vyakula duniani kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine na badala yake ameyalaumu mataifa ya magharibi kuwa chanzo cha hali hiyo. Lavrov ameyatoa matamshi hayo katika siku ya mwisho ya ziara ndefu ya kuyatembelea mataifa kadhaa ya Afrika kutafuta uungaji mkono. Akiwahutubia waandishi habari na wanadiplomasia wa Afrika kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Abbaba Lavrov kwanza ameyapinga madai ya kuwepo mzozo wa upatikanaji chakula duniani na kuitaja hali inayoshuhudiwa sasa kuwa ni mparaganyiko wa masoko ya chakula. Amekiri kuwa hali nchini Ukraine imechochea kwa sehemu fulani mparaganyiko huo lakini amesema ni hatua za vikwazo zilizochukuliwa na mataifa ya magharibi ndiyo sababu ya kutokea hali hiyo na siyo uvamizi wa Urusi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii