Wakati famili tano zilizopotelewa na watoto wao maeneo ya Kariakoo katika mazingira ya kutatanisha, wametoka tena hadharani safari hii wakimuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura kuwasaidia kuwapata vijana wao, kamanda huyo amekiri kulipokea jambo hilo na kuahidi kuwasilikiza.
IGP Wambura alisema; “nimesikia kilio chao na wakija nitawasikiliza na kulifanyia kazi suala lao kwa kuwa dhamira yetu ni kuhakikisha haki ya kila mmoja inalindwa.”
Wambura ameshika wadhifa huo, Julai 20 mwaka huu, baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akichukua nafasi ya Simon Sirro aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Hadi jana Jumatatu ni siku 211 zimepita tangu vijana hao walipotoweka katika mazingira ya kutatanisha Desemba 26 mwaka jana eneo la Kamata, Kariakoo jijini Dar es Salaam wakati wakiwa njiani na gari yao wakienda ufukweni Kigamboni kusherekea sikukuu ya Krismas.
Vijana hao waliopotea ni Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe.
Mashuhuda walidai tukio la kutekwa kwao lilitokea majira ya 11 jioni ambapo watu watatu waliokuwa wamevalia nguo zinazodaiwa za askari wakiwa katika Bodaboda waliisimamisha gari waliyokuwa wamekaa kisha kubadili muelekeo wa safari na kuondoka nao.