Maafisa wa Ukraine wamefahamisha kuwa watu 15 wameuawa baada ya majeshi ya Urusi kulishambulia kwa makombora jengo la ghorofa tano katika mji wa mashariki mwa Ukraine wa Chasiv Yar. Gavana wa jimbo la Donetsk, Pavlo Kyrylenko pia amethibitisha juu ya kuuliwa watu hao 15. Idara ya huduma za dharura imesema watu zaidi ya 24 bado wamekwama kwenye vifusi vya jengo lililoshambuliwa. Mkoa wa Donbas, ambao waasi wanaotaka kujitenga wanapigana na vikosi vya serikali ya Ukraine tangu mwaka 2014, una majimbo mawili, Donetsk na Luhansk. Wiki iliyopita, vikosi vya Urusi viliuteka mji wa Lysychansk, ngome ya mwisho iliyokuwa chini ya majeshi ya Ukraine katika mkoa wa Luhansk.