Vyombo vya habari nchini Iran vinaripoti kwamba Jeshi la Mapinduzi la Iran limewakamata wanadiplomasia kadhaa wa kigeni akiwemo Muingereza mmoja kwa madai ya upelelezi. Lakini serikali ya Uingereza kwa haraka imekanusha kukamatwa kwa afisa wake yeyote, ikidai ripoti hizo ni za uongo. Televisheni ya taifa ya Iran lakini imeripoti kwamba Muingereza huyo ajulikanaye kama Giles Whitaker, ambaye ni naibu mkuu wa mpango wa serikali ya Uingereza nchini Iran, amefukuzwa tu kutoka kwenye eneo walikokamatwa wanadiplomasia hao. Ripoti hiyo ya televisheni imemtuhumu kwa kufanya kile ilichokiita "operesheni ya upepelezi" katika maeneo ya majeshi. Ukanda mmoja wa video umeonyesha mtu aliyetambulishwa kama Whitaker akizungumza akiwa katika chumba. Serikali ya Uingereza imekanusha yote hayo. Haya yanafanyika wakati ambapo kuna mivutano mikubwa kati ya Iran na nchi zenye nguvu duniani kuhusiana na jaribio lililokwama kwa muda mrefu la kuufufua mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015. Kumekuwa pia na ongezeko la kamatakamata ya raia wa nchi za Magharibi nchini Iran.