Walioacha shule wakimbilia masomo ya uzeeni kujinusuru

WAZEE na vijana ambao hawakufanikiwa kumaliza mafunzo shuleni kaunti ya Mombasa, wamelazimika kurejea shuleni kukata kiu ya elimu.

Kulingana na Mkurugenzi wa Masomo ya Watu Wazima (CDACE) kaunti ya Mombasa Bw Franklin Karanja, umri wa wanafunzi walioamua kurudi shuleni ni kati ya 15 na 60. Anasema kila mmoja ana haja ya kuendelea alipositishia masomo ambayo yalitatizwa kwa sababu mbalimbali.

“Elimu inazidi kupata thamani kila siku. Hili limewafanya wengi kurudi shuleni. Vijana kwa wazee hawataki kukosa kazi kwa sababu hawana elimu ya msingi,” alieleza Bw Karanja.

Bw Karanja alihoji kuwa, licha ya wanafunzi wengi wa mradi huo wa masomo ya watu wazima kuwa vijana, hata wanasiasa wenye azma ya kugombea viti vya kisisasa katika siku za usoni, hawakosi kuingia darasani.

“Kuna hata wanasiasa ambao huja darasani kujiendeleza. Wengi wanataka kuboresha mawasiliano. Wengine wana nia ya kujaza pengo moja ama nyingine. Labda vyeti vya kitaaluma vya kuwasaidia kusalia katika nafasi wanayoishikilia ama ata ile wanayoimezea mate,” alisema Bw Karanja.

Bw Karanja alisema hata wafanyakazi wa umma pia hawajaachwa nyuma. Hakukosekani wanaorudi kupata elimu ili wajiendeleze kikazi.Mtaala Mpya wa Umilisi na Utendaji(CBC) pia ni chanzo cha wazazi kurejea shuleni.

Mtaala huo mpya umewapa wazazi changamoto kwani unawahusisha pakubwa katika masomo ya wanao na wengi hawataki kupata aibu.

“CBC ina kazi nyingi sana na inamtaka mzazi awe na kiasi fulani cha elimu. Kwa hivyo inambidi mzazi aje shuleni kujifunza kusoma na hata kuhesabu ili aweze kumsaidia mwanawe,” anaelezea Bw Karanja.

Kabla ya anayetaka kujiunga na masomo haya kuingia darasani, wao hufanyiwa majaribio ambayo husaidia kuwaweka katika madarasa wanayofaa.

Kwa sasa, wanafunzi 1,671 wanaendelea na masomo ya msingi huku wengine wakiendelea na masomo ya shule za msingi na za upili, katika vituo 75.

Data zinaonyesha kuwa licha ya wanawake wengi kujiunga na shule za ukubwani, wanapata taabu ya kuenda shuleni kila siku.

“Wanawake wengi ndio wanasimamia shughuli za nyumbani kwao. Hii inawafanya kutopata muda wa kutosha kuja shuleni. Kwa hivyo inatubidi tuwaombe waje hata kama ni siku tatu kila wiki,” anaelezea Bw Karanja.

Kwa sasa wanafunzi 95 ambao ni watu wazima wamejisajili kwa mtihani wa kitaifa wa shule za msingi (KCPE) utakaokaliwa Novemba, na 256 kwa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne(KCSE) utakaofanyika Desemba 2022.

Bw Karanja ana imani kuwa, watakaokali mtihani wa KCPE watafuzu na kuendelea na masomo ya shule za upili, huku wa KCSE wakifululiza hadi kwenye taasisi za masomo ya juu.

Shule hizo zinapata changamoto kadhaa ikiwemo, ukosefu wa walimu wa kutosha wa kuwahudumia wanafunzi. Alielezea kuwa, ukosefu wa miundo misingi ya kutosha unaathiri utendakazi wa CDACE.

Shida nyingine ni ukosefu wa pesa za kulipia tozo za kukalia mitihani ya kitaifa.

Bw Karanja alishukuru maeneobunge ya Nyali na Changamwe kwa kujitolea kuwalipia wanafunzi wao karo na tozo za mitihani ya kitaifa kupitia hazina ya maendeleo ya maeneobunge (CDF).

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii