Afisa wa polisi afariki akikabiliana na mhalifu

AFISA wa polisi aliuawa kwa kufyatuliwa risasi na mshukiwa wa ujambazi wakati maafisa wa polisi walikuwa wakiingia katika nakazi ambako mshukiwa alikuwa amejificha.

Aidha, afisa mwingine wa polisi alipelekwa hospitalini akiwa na jeraha la risasi begani baada ya kufikiwa na risasi katika patashika hiyo ya ufyatulianaji risasi.

Baada ya zaidi ya saa mbili za makabiliano, mshukiwa aliuawa na polisi kwa kumiminiwa risasi alipoingia ndani ya shimo la choo.

Isitoshe, polisi walipata bastola aina ya Ceska ikiwa na risasi tatu (9mm) kutoka kwa mshukiwa, wakapata bunduki ya kujitengenezea ikiwa nyumbani kwa mshukiwa na pia kumkamata rafiki ya mshukiwa kwa jina Bi Scholastica Nduku, 20.

Mbali na hayo, simu kadhaa, kadi za simu zilizoaminika kuibwa katika duka moja mtaani South B zilipatikana zimefichwa chini ya godoro. Pia maafisa walitwaa mali ya wizi iliyoibwa kutoka kwa Kenya Power.

Mkuu wa polisi katika eneo la Makadara, Bw Timon Odingo alisema kisa hicho kilitokea usiku wa kuamkia Jumanne katika eneo la Kamae, mtaani Kahawa West, kaunti ndogo ya Roysambu, Kaunti ya Nairobi.

Bw Odingo alisema afisa aliyeuawa alikuwa ni Sajini Gravous Osieno aliyehudumu katika kituo cha polisi cha Lunga Lunga.

Mshukiwa alitambuliwa kwa jina Ibrahim Waweru Wagechi kwa jina la utani ‘Mwarabu’, 23.

“Alikuwa ndani ya orodha ya wahalifu sugu. Tumemsaka kwa udi na uvumba baada ya kufanya msururu wa uhalifu Nairobi. Tulikuwa na habari kwamba ameingia nyumbani anakojificha,’’ Bw Odingo akasema.

Kadhalika, Bw Odingo aliongeza kwamba kilikuwa kibarua kigumu kumpiga risasi mshukiwa akiwa ndani ya shimo.

Hata hivyo, maafisa wake wakishirikiana na wenzao kutoka Roysambu na wengine kutoka Kasarani walifanikiwa kumuua.

“Kikosi cha maafisa wa Makadara kiliungani na vikosi zaidi wakiwemo polisi wa Roysambu na wenzao wa kutoka Kasarani,” Bw Odingo akaeleza.

Baada ya mshukiwa kuuawa, polisi waliingia ndani ya shimo na kutoa mwili wakitumia kamba.

Baada ya kukosa bastola kutoka kwa mshukiwa, polisi waliagiza waletewe jenereta ili wapige maji kutoka ndani ya shimo.

Hata baada ya bidii yote kuwepo, polisi hawakufanikiwa kupata silaha ndiposa wakapea vijana kibarua cha kuzoa matope yaliyokuwa ndani ya choo.

“Japo mwenye ploti hakuwa amejenga choo. Mshukiwa alikuwa amedungwa mwilini na vyuma vilivyokuwa ndani ya shimo. Ilibidi tutumie jenereta kutoa maji yote tukitafuta bunduki,” Bw Odingo akaendelea.

Hatimaye, maafisa wake walipata bastola aina ya Ceska ikiwa na risasi mbili pamoja na risasi ya tatu iliyokuwa imetumika ndani ya matope.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii