Mshukiwa wa wizi auawa mtaani South B polisi wakifanikiwa kutwaa bastola

MAAFISA wa polisi walitibua mpango wa wizi wa mabavu katika jengo moja mtaani South B katika kaunti ndogo ya Starehe usiku wa kuamkia Jumapili.

Mshukiwa mmoja aliuawa kwa kufyatuliwa risasi na polisi huku wenzake wawili wakifanikiwa kutoroka.

Aidha, polisi walipata bastola aina ya Browning ikiwa na risasi tatu.

Mkuu wa polisi katika eneo la Makadara, Bw Timon Odingo alisema

“Washukiwa wote walikuwa wamebebwa na pikipiki wakati wa usiku lakini maafisa wangu walikuwa wamejipanga na kuwangojea wakizingira jengo lenyewe,” Bw Odingo akasema.

Bw Odingo aliongeza kwamba maafisa wengine wa polisi waliwasubiri washukiwa hao wakiwa ndani ya gari lao lililosimamishwa gizani.

“Kwa sababu tulikuwa na habari kuwahusu, polisi wengine waliwasubiri ndani ya gari lao lililozimwa taa. Washukiwa walipokaribia jengo hili, polisi waliwasha mataa ya gari ghafla wakimlika pikipiki na kusababisha mwendeshaji pikipiki kukosa mwelekeo,” akasema.

Katika pilkapilka hizo, mshukiwa mmoja alianguka barabarani na ndipo ufyatulianaji mkali wa risasi ukaanza.

Mshukiwa mmoja aliilenga risasi gari la polisi aina ya Subaru na kumiminia magurundumu yake risasi na kuyatoa pumzi.

Polisi nao walijibu kwa kumlenga mshukiwa huyo na kufanikiwa kumuua akifariki papo hapo huku wenzake wakitorokea katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Shimo la Tewa.

Polisi walichukua bastola ya mshukiwa na kuipeleka katika ofisi za DCIO ili ikaguliwe nao mwili wa mshukiwa aliyeuawa ukipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City.

Baada ya uchunguzi wa wataalamu wa bunduki, ilibainika bastola hiyo ilitumiwa kutekeleza uhalifu katika mitaa ya Buruburu, Pipeline na maeneo ya Embakasi.

“Tulipata kwamba silaha hiyo ilikuwa imetumika katika visa vya uhalifu Buruburu, Pipeline na katika maeneo ya Embakasi,” Bw Odingo akaongeza.

Katika siku za hivi karibuni, uhalifu wa ujambazi katika eneo la Makadara umeenda chini ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.

Ili kufanikisha juhudi hizo, kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Makadara, Bw Timon Odingo na naibu wake Bi Judith Nyongesa wamebuni mikakati mipya ya kukabiliana na uhalifu.

“Nimebadilisha kikosi changu kwa kuwaweka maafisa wapya waliopewa jukumu la kutibua mipango yote ya wahalifu kabla ya kutenda maovu katika jamii. Vile vile tumeimarisha ushikaji doria, na kambi nazo ni nyingi tukiongeza vituo vitano vya polisi,” Bw Odingo akadokeza.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii