Akaunti za Twitter na Youtube za Jeshi la Uingereza Zadukuliwa, Jeshi Kufanya Uchunguzi

AKAUNTI za mitandao ya kijamii ya Twitter pamoja na Youtube za Jeshi la Uingereza zimedukuliwa na watu wasiojulikana huku zikionesha baadhi ya maudhui ya sarafu za mtandaoni (cryptocurrency) pamoja na picha za bilionea namba moja duniani, Elon Musk.

 

Katika ukurasa rasmi wa jeshi hilo Twitter, ilionesha kuchapishwa baadhi ya maudhui yanayohusiana na biashara ya sarafu za mtandaoni, kitu ambacho ni kinyume na maudhui ya jeshi hilo.

 

Jeshi la Uingereza limethibitisha kuwa linachukulia kwa unyeti usalama wa taarifa zake na lilikuwa katika mchakato wa kutatua tatizo hilo na kuthibitisha kuwa akaunti zote zimefanikiwa kurejeshwa.

Msemaji wa Jeshi la Uingereza amenukuliwa akisema: “Ingawa changamoto imeshatatuliwa lakini uchunguzi unaendelea na haitakuwa sahihi kusema chochote kwa wakati huu ambao tunaendelea na uchunguzi.”

Hadi sasa haifahamiki nani ambaye yupo nyuma ya mchakato huo wa udukuzi huo uliosababisha hadi kubadilishwa kwa majina ya akaunti hizo.

Kwa wakati fulani, jina la akaunti ya jeshi hilo ya Twitter lilibadilishwa na kuitwa Bapesclan ikiambatana na picha ya katuni iliyovaliwa taji la kifalme.

Mbunge wa Chama cha Conservative na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Bunge alisema: “Tatizo linaonekana kuwa kubwa. Natumaini matokeo ya uchunguzi na hatua stahiki zitachukuliwa.”

Si mara ya kwanza kwa akaunti za watu au taasisi zenye majina makubwa kuathirika mnamo mwaka 2020 akaunti nyingi kubwa nchini Marekani zilidukuliwa na kuhusishwa na biashara ya Bitcoin.

Akaunti zilizoathiriwa ni pamoja na ya Elon Musk, Joe Biden, Jeff Bezos, Barack Obama, Bill Gates na Kanye West.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii