Wahausa waitisha maandamano mjini Khartoum leo Jumanne

Maelfu ya watu kutoka kabila la Hausa nchini Sudan wameweka vizuizi barabarani na kuzichoma moto ofisi za serikali, baada ya makabiliano makali ya kikabila katika jimbo la Blue Nile. Kufuatia makabiliano hayo ya wiki nzima yaliyouwa watu wasiopungua 79, wanaharakati wa Kihausa wameitisha maandamano mjini Khartoum leo Jumanne ili kuzimulika ghasia hizo. Mtu maarufu kutoka jamii ya Hausa ameliambia shirika la habari la AFP kuwa uhasama ulizuka baina ya makabila ya Hausa na Berti mwanzoni mwa wiki iliyopita, baada ya Waberti kukataa ombi la Wahausa kutaka iundwe mamlaka ya kiraia ya kusimamia umiliki wa ardhi. Hata hivyo, Waberti wanasema walichokifanya ni kujibu mashambulizi ya Wahausa kwenye ardhi yao. Haya yanajiri licha ya gavana wa jimbo la Blue Nile, Ahmed al-Omda kupiga marufuku maandamano na kuweka amri ya kutotoka nje usiku kwa kipindi cha mwezi mzima.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii