Chama tawala katika Jamhuri ya Congo kimeripoti kushinda katika uchaguzi wa bunge wa wiki iliyopita.Matokeo ya awali yaliyotangazwa kwenye televisheni ya taifa yanaonyesha chama cha Labour cha Congo - PCT kilishinda viti 103 kati ya viti 151 vya bunge. PCT ni chama cha Rais Denis Sassou Nguesso, mwanajeshi wa zamani mwenye umri wa miaka 78 ambaye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza katika taifa hilo la Afrika ya kati mwaka 1979. Vyama vidogo vinavyoshirikiana na PCT vilishinda viti 13, kulingana na matokeo ya awali. Hata hivyo, makundi ya upinzani yameyataja matokeo hayo kuwa ya udanganyifu. Duru ya pili ya kura iliyopangwa kufanyika Julai 24 itaamua kuhusu viti 27 vya bunge ambavyo havijajazwa.