Waasi waua wanakijiji 7 Jamhuri ya Afrika ya Kati

Kundi la waasi limewashambulia na kuwaua wanakijiji 7 kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, taifa ambalo linaandamwa na vita kwa miaka kadhaa.Duru za polisi kwenye eneo hilo zimesema washambuliaji kutoka kundi la 3R moja ya makundi makubwa ya watu wenye silaha nchini humo walikivamia kijiji cha Ndanga karibu na mpaka wa taifa jirani la Chad na kuwashambulia watu.Mwanasiasa mmoja kutoka mji wa jirani wa Ngaoundaye ameliambia shirika la habari la AFP kuwa washambuliaji walifyetua risasi ovyo zilizowauwa watu 7 na kuwajeruhi watu wengine 6.Inaarifiwa kuwa washambuliaji hao wamemchukua mateka mwanamume mmoja walipokuwa wakitoroka pale wanajeshi walipowasili eneo la tukio. Mkasa huo ni mwendelezo wa hujuma za makundi ya waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo imetumbukia kwenye vita na machafuko ya kisiasa katika kipindi cha miaka tisa iliyopita.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii