Marekani yalaani matamshi ya kumdhihaki mtume Mohammed

Marekani imelaani vikali matamshi yaliyotolewa na maafisa wa chama tawala nchini India cha BJP kuhusu mtume Mohammed ambayo yamezusha hasira na ukosoaji mkubwa kutoka mataifa ya kiislamu.Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Marekani Ned Price amesema Washington inakosoa vikali matamshi hayo ya maudhi yaliyotolewa na maafisa wawili wa chama cha BJP na imefarijika kuona chama hicho pia kimelaani suala hilo.Mnamo Mei 26 msemaji wa chama hicho cha waziri mkuu Narendra Modi, Nupur Sharma alitoa matamshi yaliyotafsiriwa kudhihaki ndoa ya mtume Mohammed na mkewe mdogo Aisha ambayo yameughadhibisha umma wa waislamu duniani.Katika kujibu suala hilo chama chake kilitangaza kumsimamisha kazi Nupur pamoja na mwanachama mwengine Naveen Kumar aliyetuhumiwa kuandika ujumbe wa kumchafua Mtume Mohammed kupitia ukurasa wa Twitter.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii