Mkosoaji wa serikali ya Urusi aliyefungwa jela, Alexei Navalny, amesema amehamishiwa kwenye kile kinachotajwa kuwa moja ya gereza la kutisha zaidi nchini humo. Kupitia ukurasa wa Instagram, Navalny mwenye umri wa miaka 46 ameandika amehamishiwa katika kizuizi kikali cha Melekhovo na kwamba kwa hali hiyo hana la kuongeza zaidi. Mwezi uliopita, mpinzani huyo mkubwa kabisa wa Rais Vladimir Putin, akiwanukuu wafungwa wengine alisema serikali ya Urusi inamtayarishia gereza ndani ya gereza. Navalny amekuwa akitumikia kifungo cha miaka miwili na nusu katika gereza la mji wa Pokrov, kilomita 100 mashariki mwa Moscow, kwa kukiuka masharti ya msamaha wake katika mashtaka ya zamani ya ulaghai katika kile washirika wake wanasema ni adhabu iliyotokana na kuipinga serikali.