Uingereza yasitisha zoezi la kuwahamisha waomba hifadhi kwenda Rwanda

Serikali ya Uingereza imelazimika kufuta safari ya kundi la kwanza la wahamiaji waliotarajiwa kuwasili nchini Rwanda hivi leo, baada ya agizo la Mahakama ya Haki za binadamu ya bara Ulaya.


Uamuzi huo wa Mahakama ni pigo kwa serikali ya Uingereza, ambayo siku ya Jumanne ilikuwa imeandaa ndege ya kuwasafirisha kundi la Kwanza la wahamiaji saba nchini Rwanda. 

Hata hivyo, ni ahueni kwa wahamiaji hao na watetezi wa haki za binadamu ambao wamekuwa wakipinga mpango huu wa serikali ya Uingereza na Rwanda. 

Waziri wa Mambo ya ndani wa Uingereza Priti Patel licha ya kusikitishwa na uamuzi wa agizo la kufutwa kwa safari ya Jumanne, anasema serikal bado iko mbioni kuhakikisha kuwa wahamiaji hao wanapelekwa Rwanda, huku Waziri Mkuu Boris Johnson akieleza umuhimu wa mpango huo. 

Nchini Rwanda, serikali inasema iko tayari kuwapokea wahamiaji hao kutoka Uingereza na inasisitiza inafanya hivyo kwa sababu za kibinadamu wala sio kwa sababu za kifedha kulingana na Mukuralinda Alain naibu msemaji wa serikali. 

Tangu mwezi Aprili, wakati Uingereza na Rwanda zilivyotia saini mkataba huo, wanaharakati wa haki za binadamu, viongozi wa dini na hata Mwanamfalme Charles walipinga mpango huo, wakisema ni kinyume cha haki za binadamu huku wengine wakisema Rwanda sio nchi salama kwa wakimbizi hao.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii