Khalwale afukuzwa kikaoni kwa kuvumisha mwaniaji wa ODM

VURUGU zilitokea katika mkutano wa kampeni wa Muungano wa Kenya Kwanza katika Kaunti ya Kakamega, baada ya wafuasi wa Seneta Cleophas Malala kumfurusha seneta wa zamani, Dkt Boni Khalwale, wakimsuta kwa kumpigia debe mgombea ugavana kwa tiketi ya ODM, Fernandes Barasa.

Uhasama kati ya wanasiasa hao ulitokea katika mkutano huo uliofanyika katika soko la Mandere, eneo bunge la Matungu, Jumanne jioni.

Dkt Khalwale aliuambia umati kwamba, alipohudumu kama Mbunge na Seneta, alitambuliwa kwa kazi nzuri miongoni wa wajumbe wote nchini nyakati hizo.

Video iliyowekwa mitandaoni ilimwonyesha Seneta Malala akimkosoa Dkt Khalwale kuhusiana na kauli yake kuhusu kinyang’anyiro cha ugavana Kakamega.

Dkt Khalwale ambaye alijiondoa kutoka kinyang’anyiro cha ugavana mnamo Machi 2022 na kuahidi kumuunga mkono Seneta Malala alisema: “Mimi ni Khalwale. Nataka ujue kwamba mimi Khalwale, Malala na Fernandes Barasa ni watoto wamoja kutoka Kakamega. Tunapigania uongozi ili kuwahudumia. Mwafaa kumchagua kiongozi bora atakayewahudumia.”

Seneta Malala alikasirika kwamba, Dkt Khalwale alifeli kuidhinisha azma yake ya ugavana katika mkutano huo.

Dkt Khalwale akaongeza: “Mimi ndiye mbunge bora zaidi kuwahi kuhudumu katika historia ya Kenya. Mungu awabariki.”

Kauli hiyo ilionekana kumkasirisha Seneta Malala ambaye aliwaambia wafuasi wake kwamba, Dkt Khalwale alionekana kuchanganyikiwa.

“Anatwambia nini? Je, amechanganyikiwa?” akauliza Seneta Malala akirejelea kauli za Dkt Khalwale.

“Anafaa kufahamu kwamba, hapa ni ngome yangu na nitashinda kiti cha ugavana,” akasema Bw Malala.

Kisha akapaza sauti kwa kusema: “Cleo ndiye Gavana!”

Hapo ndipo wafuasi wake walianza kuimba, “Khalwale aende! ! Khalwale aende!”

Fujo ziliposambaa, Dkt Khalwale alilalizimika kuondoka haraka kwa gari lake huku vijana wakimzomea kwa maneno makali.

Baadhi ya vijana walishambulia gari hilo kwa mawe.

Dkt Khalwale ametoa  kauli zake katika mkutano huo zilieleweka visivyo.

“Tulikuwa katika ngome ya mmoja wa wapinzani wetu na hatungemshambulia kwa maneno makali. Tunashirikiana katika Kenya Kwanza lakini mwenzangu Bw Malala anaonekana kuvuruga ushirikiano huo,” akasema.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii