Mwanamke asakwa kwa madai ya kuhepa na gari la mpenzi

POLISI wanamsaka mwanamke aliyetoroka na gari la mpenzi wake baada ya wawili hao kuwasili katika mji wa Naivasha kubarizi.

Kulingana na rekodi za polisi, wawili hao waliwasili Naivasha Jumamosi kutoka Narok na kuanza kujiburudisha kabla ya mwanamke huyo kutoweka na kumuacha mpenzi wake.

“Mwanamume huyo aliripoti kisa hicho na pia akadai kwamba alikuwa ameweka zaidi ya Sh700,000 ndani ya gari hilo,” duru ndani ya polisi zilisema.

Mwanamke huyo anayesemekana kuwa na umri wa miaka 40, aliondoka bila mwanamume huyo aliyekuwa amepata pesa baada ya kuuza ngano.

“Tunataka kubaini jinsi mwanamke huyo aliweza kutoroka au iwapo mwanamume huyo alileweshwa kabla ya tukio hilo,” duru katika polisi iliongeza.

Mwanamume huyo alienda katika kituo cha polisi cha Naivasha baada ya kukosa kumpata mwanamke huyo aliyepanga kujivinjari naye.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii