Mahakama ya Senegal imemuhukumu kiongozi wa waasi kifungo cha maisha jela kwa mauaji

Mahakama nchini Senegal Jumatatu ilimhukumu kiongozi mtoro wa waasi na wanaume wengine wawili kifungo cha maisha jela kwa mauaji pamoja na uasi wa kutumia silaha kutokana na mauaji yaliyogharimu maisha ya watu 14.

Cesar Atoute badiate mkuu wa Movement of Democratic Forces of Casamance (MFDC) kundi la waasi linalopigania uhuru katika eneo la kusini mwa Senegal alihukumiwa bila yeye kuwepo kufuatia mauaji hayo.

Omar Ampoi Bodian mwanachama mwingine wa kundi hilo na mwandishi wa habari Rene Captain Bassene walipewa hukumu hiyo-hiyo wakili wao Cire Cledor Ly aliliambia shirika la habari la AFP.

Mahakama ya Ziguinchor katika jiji kuu la Casamance ilitoa hukumu zilizosimamishwa kwa miezi sita kwa washtakiwa wengine wawili na kuwaachilia wengine 11. Kesi hizo zilitokana na tukio la Januari sita mwaka 2018 ambapo wanaume 14 walifungwa kamba na kuuawa wakati walipokuwa wakienda kukata kuni katika msitu uliohifadhiwa karibu na Ziguinchor.

Wapiganaji wa waasi wa Casamance walitumia msitu huo kama kituo na mamlaka ya Senegal inawashutumu kwa kufadhili shughuli zao na kusafirisha kuni pamoja na bangi. Kundi hilo la waasi lilikanusha kuhusika kwa vyovyote vile likiwashutumu maafisa wa serikali kwa ufisadi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii