Watu takriban 19 wamepoteza maisha na wengine 12 wamejeruhiwa katika ajali ya basi la abiria lililoteleza na kutumbukia kwenye korongo la kina kirefu katika barabara ya milimani kusini magharibi mwa Pakistan.Mahtab Shah naibu kiongozi wa wilaya ya Shirani amesema takriban abiria 35 walisafiri na basi hilo na kuongeza kuwa waokoaji waliendelea na zoezi la kutafuta manusura katika mabaki ya gari lililoharibika vibaya na kwenye eneo ilipotokea ajali hiyo.Nchini Pakistan ajali za barabarani zimekuwa zikitokea mara kwa mara kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara, kutozingatiwa kwa sheria za barabarani pamoja na kuchakaa kwa magari. Mwezi uliopita watu takriban 22 walipoteza maisha kwenye ajali ya basi lililopinduka na kutumbukia kwenye korongo.