Marekani yafungua uchunguzi baada ya wahamiaji 51 kufa kwa joto ndani ya Trela

Idadi ya vifo vya wahamiaji wasio na vibali waliotelekezwa kwenye trela lenye joto kali mjini Texas imepanda hadi 51 jana Jumanne, huku Rais Joe Biden akiwalaumu wale aliowaita wahalifu wenye utaalamu wa kusafirisha binadamu kimagendo kwa janga hilo. Afisa wa Kaunti ya Bexar Rebeca Clay-Flores, aliripoti idadi mpya ya maiti za wanaume 39 na wanawake 12 kufuatia ugunduzi wa Jumatatu, wa trela kwenye barabara isiyotumiwa sana katika wilaya yake. Wizara ya usalama wa ndani ilitangaza kuwa imeanzisha uchunguzi wa uhalifu juu ya kisa hicho. Maafisa wa sheria kutoka serikali kuu ya Marekani jana Jumanne waliwakamata wanaume wawili kutoka anuani iliyohusishwa na usajili wa trela hilo, kwa mujibu nyaraka za mahakama. Kwa mujibu wa rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador, miongoni wa marehemu ambao utambulisho wao unajulikana, 22 walikuwa raia wa Mexico, saba kutoka Guatemala na wawili kutoka Honduras.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii