Idadi ya watoto waliokufa kutokana na mitetemeko ya ardhi imeongezeka na kufikia 155

Umoja wa Mataifa umesema idadi ya watoto waliokufa kutokana na mitetemeko ya ardhi nchini Afghanistan sasa imefikia 155. Asasi ya misaada ya Umoja huo, OCHA imesema watoto wengine wapatao 250 wamejeruhiwa. Idadi kubwa ya watoto walikufa kwenye eneo la Gayan lililokumbwa zaidi na mitetemeko hiyo ya ardhi. Wataliban wanaotawala nchini Afghanistan wamesema idadi ya watu waliokufa hadi sasa inafikia 1,150. Kwa mujibu wa watawala hao watu wengine zaidi ya 700 wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa taarifa zaidi watoto wapatao 65 wamekuwa yatima. Maafa ya tetemeko la ardhi yatapima uwezo wa utawala wa kundi la Taliban, mbali na matatizo ya umasikini, njaa na changamoto za kiuchumi. Baada ya Marekani na washirika wake kuondoka Afghanistan misaada ya kimataifa ilisimamishwa kwa ajili ya nchi ya Afghanistan.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii